JUUKO, MKUDE WANAWEZA KUWA WAOKOZI WA SIMBA





Na Saleh Ally
UNAWEZA kuona kama Simba wameshapiga hatua baada ya kukusanya pointi tatu za kwanza katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini uhalisia unaonyesha kazi yao imezidi kuwa ngumu.

Simba wamewafunga JS Saoura kwa mabao 3-0 na kufanikisha kupata pointi hizo tatu, lakini wameamsha morali kuu. Hili ni jambo zuri kwao unapozungumzia hesabu sahihi za kiushindani.

Kiuhalisia, Simba bado wana kazi kubwa sana na lazima wafanye kazi ya ziada kuhakikisha wanafika mbali.

Hesabu za uhakika zitatokana na mwendo wanaotaka kwenda kwa kuwa ugumu unakwenda kuongezeka. Maana wanakutana na timu ambazo unaziona ndizo zinapewa nafasi ya kwanza na pili kwenye kundi kwa maana ya rekodi.

Mara nyingi timu zimefanikiwa kuvunja rekodi za awali lakini mara nyingi timu zimeshindwa kabisa kuzing’oa timu zenye rekodi nyingi.

Kwa maana ya ubora na uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa, Al Ahly lazima itakuwa namba moja, AS Vita ya DR Congo inafuatia na baadaye ni Simba, halafu Saoura ya Algeria ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo.

Simba inaweza kupita na kupata nafasi dhidi ya wazoefu hao lakini kazi lazima iwe ngumu isiyo na kifani.



Kawaida unapotaka kuwa bora, lazima upambane na walio bora kufikia kiwango hicho. Simba itaweza lakini lazima kutakuwa na ugumu zaidi.

Mechi dhidi ya AS Vita kesho Jumamosi, itakuwa ngumu kwa kuwa uchezaji wa timu hiyo ya DR Congo unabadilika sana kutokana na timu na kikubwa ambacho kitawasumbua Simba ni aina ya uchezaji inayotaka kufanana kwa asilimia kubwa.

Faida ya Wakongo hao wanacheza kwa kasi kubwa. Pasi zao ni za kuachiana na kila upande unakwenda kwa mwendo ambao Simba watalazimika kuwa makini sana katika safu ya ulinzi.

Nimeona katika mechi yao dhidi ya Al Ahly, licha ya kupoteza kwa mabao 2-0, Wakongo hao waliendelea kumiliki mpira na kushambulia kwa kasi.

Kumbuka walikuwa pungufu baada ya mchezaji mmoja kulambwa kadi nyekundu, lakini pia wako ugenini. Sasa watakuwa nyumbani na kawaida mashabiki wao hujitokeza kwa wingi sana na kufanya uchezaji wao uwe ule wa hamasa.

Kikubwa kabisa kwa Simba kuna mambo lazima wayafanyie kazi hiyo kesho au kuyaboresha zaidi.

Mkude:
Kama haukuangalia vizuri mechi iliyopita dhidi ya Saoura, unaweza kutofautiana sana na mimi. Lakini nisikilize vizuri sana.

Jonas Mkude hakuwa katika kiwango kizuri kama ambavyo alicheza katika mechi dhidi ya Nkana hasa ile ya ugenini nchini Zambia.

Kuwa katika kiwango kisichofanana na wenzake, mzigo zaidi umekuwa ukimuangukia kiungo mwingine, James Kotei ambaye analazimika kufanya kazi ya ziada.

Kwa uchezaji wa AS Vita, kama Mkude atacheza chini ya kiwango, Kotei hataweza kuhimili. Hii itamlazimisha Clautus Chama kushuka chini na kuifanya Simba ishindwe kuchezea mpira juu kwa maana ya kushambulia.

Hivyo lazima Mkude awe ameambiwa, naye awe amekubalina na kulifanyi kazi.

Unapokutana na timu yenye kiungo bora, halafu ukawa una kiungo dhaifu, basi ujue umeumia.

PEMBENI:
Mwendo wa AS Vita ni kasi, katikati zaidi wanamtumia yule rasta aliyevaa jezi namba 14. Kama Simba watamdhibiti katika kiungo kutokana na ubora wake basi wategemee mfumo mpya.

Mfumo wa pili wa AS Vita ni kushambulia kupitia pembeni kwa winga na mabeki wake wa pembeni.

Maana yake, Nicholaus Gyan na Mohammed Hussein lazima wajiandae katika suala la kupata shida kwa kuwa rasta ana uwezo wa kupiga pasi nyingi ndefu zinazofika.

Krosi nyingi, zina wamaliziaji wazuri na Wakongo wengi huwa wazuri katika upigaji vichwa.

JUUKO:
Usisahau faulo nyingi za Juuko Murshid Simba ikiwa inakaba. Ninaamini zikiendelea zitakuwa na madhara makubwa kwa ugenini.

Kama Juuko atakuwa akicheza “kisela” kama mechi iliyopita kuna hasara mbili ziko tayari na zinaweza kuikumba Simba.

Hasara ya kwanza ni Juuko kupata kadi ya njano na Simba kucheza pungufu. Ikiwa hivyo maana yake muda mwingi watalazimika kulinda badala ya kushambulia.

Hasara ya pili ni faulo karibu na lango, AS Vita wana wapigaji wazuri wa mipira iliyokufa. Hivyo hili nalo ni tatizo wanalopaswa kuliangalia.

Baada ya hapa, Simba wanaweza kuangalia sasa wafanye nini kupata mabao, jambo ambalo wanaliweza na rekodi zinawabeba.




from SALEH JEMBE http://bit.ly/2CsmS4y
ILI KUWA WA KWANZA KUPATA HABARI USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON