Nimpongeze Rais Magufuli kwa kuhakikisha anairejesha nchi kwenye misingi - Waziri Mkuu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameutaka uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuona namna bora ya kuhuwisha mitaala ya Chuo hicho ili kifikie viwango vya Elimu ya Juu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo amesema mpaka sasa Chuo hicho kimekidhi viwango vya kuwa na hadhi ya Chuo Kikuu na kwamba elimu inayotolewa katika chuo hicho ndio inasisitizwa nchini.
Ameutaka uongozi wa chuo hicho kutia mkazo katika mafunzo ya uongozi na maadili hususan yale yenye mwelekeo wa kujenga uzalendo na kuendelea kutumia fursa ya uwepo wa makongamano kukuza uelewa wa jamii ya watanzania kuhusu umuhimu wa kuenzi falsafa za mwalimu katika umoja, upendo, uzalendo, uadilifu na mshikamano wa kitaifa.
Aidha Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kujenga misingi ya Amani, umoja na kuleta maendeleo ya jamii nchini kwa vitendo na kuwataka watanzania kuzingatia maadili, uzalendo na utaifa katika uwajibikaji wa kila siku, kuungana kwa pamoja bila kujali itikadi za kisiasa au kabila katika kulinda na kudumisha tunu hizo.
“Nimpongeze Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi anazochukua ili kuhakikisha anairejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya awali ambayo ni kuwa na viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kulinda Amani na kudumisha umoja katika jamii, watanzania wote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi na kuzilinda kwa nguvu zote,” alisema Mhe. Majaliwa.
Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Ndalichako amesema ni vizuri kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa ni mtu ambaye amelipigania Taifa na kuliletea ukombozi na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufuata nyayo za Baba wa Taifa.
Chanzo MUUNGWANA BLOG
ILI KUWA WA KWANZA KUPATA HABARI USISAHAU KU LIKE PAGE YETU,BONYEZA LIKE BUTTON
